Hifadhi ya Mazingira Asilia Chome/Shengena inasimamiwa na Wakala wa Huduma
za Misitu Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Hifadhi hii ilitangazwa katika tangazo la Serikali (GN) Na. 125 la tarehe
25/05/1951 kama msitu wa Hifadhi. Baadaye hifadhi hii ilipandishwa hadhi na
kuwa Hifadhi ya Mazingira Asilia kwa tangazo la Serikali Na. 105 la tarehe
25/03/2016. Hifadhi ina ukubwa wa hekta 14,283 na urefu wa mpaka upatao
Kilometa 67. Hifadhi inazungukwa na vijiji 27, kata 11 ambapo wakazi wake kwa
kiasi kikubwa maisha yao hutegemea uwepo wa hifadhi ya Chome kwa shughuli za
kiuchumi na kijamii. Hifadhi hii ina umuhimu mkubwa Kitaifa na Kimataifa
kutokana na vyanzo vingi vya maji vilivyopo na utajiri mkubwa wa bioanuwai.
Katika kuhakikisha kuna usimamizi mzuri, hifadhi ya mazingira asilia ya Chome
imegawanyika katika maeneo (Safu) matano ya usimamizi ambayo ni Chome, Suji, Mamba
myamba, Bombo na Bwambo.
2.0 MALENGO
Hifadhi
hii imeanzishwa ikiwa na malengo yafuatayo:
1 .Kutunza mazingira asili, mifumoikologia katika
uasilia wake.
2. Kuimarisha uhifadhi wa baioanuwai na mifumoikolojia.
3. Kuimarisha mafunzo na tafiti mbalimbali.
4. Kushirikisha jamii na wadau wote katika
kulinda, kuhifadhi na kuendeleza
uhifadhi.
5. Kuelimsha jamii inayozunguka hifadhi njia
mbadala ya kujiongezea kipato katika kupunguza umaskini na kupunguza utegemezi
wa hifadhi
3.0 UMUHIMU WA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA YA CHOME
Hifadhi ya mazingira asilia ya chome ni hifadhi yenye umuhimu wa kipekee siyo
tu kwa wakazi wa wilaya ya Same bali pia hata kwa Taifa kwa ujumla. Hifadhi hii ina
umuhimu ufuatao:-
·
Eneo hili lina bio-anuwai nyingi za mimea na wanyama(ndwele/adimu). wanaopatikana katika hifadhi hii pekee .
mojawapo ya ndege ndwele anaitwa “South Pare white eye” .
Picha 1: South Pare White eye. Picha 2: Black and white colobus
monkey
·
Hifadhi hii, ni kivutio cha utalii wa
wanyama, ndege, maporomoko ya maji, maumbile asilia, mimea adimu nk.
·
Eneo hili linatunza maumbile ya asili, kuboresha hali ya hewa na kuhifadhi gesi ukaa
na kuvuta mawingu yanayoleta mvua za mara kwa mara.
·
Hifadhi
hii ni chanzo cha maji kwa matumizi ya kilimo na chakula kwa jamii na wakazi
wanaozunguka hifadhi hii
4.0 SHUGHULI ZINAZOTEKELEZWA NA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA YA CHOME
Ili kuhakikisha kuwa uhifadhi unaendelea na hatimaye kufikia malengo na
umuhimu tajwa hapo juu hifadhi hii inafanya
shuguli zifuatazo;
·
Kufanya Doria shirikishi
ndani na nje ya Hifadhi kwa kushirikiana na Kamati za Maliasili za vijiji.
·
Kuimarisha mpaka wa
hifadhi kwa kusafisha mipaka na kupanda miti kwa lengo la kuepuka wavamizi wa
hifadhi na kudhibiti matukio ya moto.
·
Kurejesha maeneo
yaliyoharibiwa na wachimbaji madini haramu kwa kufukia mashimo yaliyoachwa
wazi, kurudisha mikondo ya maji kwenye njia za asili na kupanda miti.
·
Kuimarisha miundo mbinu
ya kitalii kwa ajili ya utalii ikolojia.
·
Kuiwezesha jamii inayozunguka
hifadhi kuanzisha bustani zao za miti
kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao.
·
Kuiwezesha jamii
inayozunguka hifadhi kuanzisha miradi
midogomidogo ya kujiongezea kipato mfano ufugaji nyuki,ufugaji wa vipepeo,
ufugaji wa samaki , ufugaji wa kuku n.k.
·
Kushirikisha jamii katika shughuli za uhifadhi
na utunzaji wa mazingira kwa ujumla
·
Kuandaa mipango ya
utekelezaji kazi, usimamizi wa hifadhi na sheria ndogondogo za vijiji
·
Kutengeneza mabango
yanayoelezea eneo la hifadhi na kuyasimika
katika mipaka ya hifadhi
·
Kuweka maboya kwenye
mpaka wa hifadhi ili kudhibiti wahalifu kutoka nje ya hifadhi ya asilai ya Chome
5.0 FULSA ZA HIFADHI YA
CHOME KWA WANANCHI NA JAMII
(a)
UTALII : Katika kuongoza watalii, wananchi wanapata kipato kwa
kuongoza watalii, mfano kata ya Chome wananchi wamenufaika kwa kutembelewa na
watalii katika nyumba zao na kuona jinsi wanavyoishi kulingana na tamaduni za Kipare.
Aidha watalii wameweza kufadhili baadhi ya watoto wa jamii kuwasomesha shule
(b)
UWEKEZAJI: Kuna fursa za kuwekeza kwenye hifadhi kama kujenga
hoteli za kitalii, ufugaji nyuki,ufugaji vipepeo, uwekezaji wa kuanzisha umeme
mdogo kwenye maporomoko ya maji ndani na nje ya hifadhi, uwekezaji wa ujenzi wa
viwanda vidogo vya maji ya kunywa nk. Aidha wakati wa kujenga miundo mbinu ya
utalii mfano hoteli, wananchi wamepata ajira.
(c)
AJIRA: Wananchi wamekuwa na wataendelea kuajiriwa kwa kazi za
usimamizi wa hifadhi mfano ufyekeaji wa mipaka ya misitu, usimikaji wa maboya (beacons),
parizi za barabara ndani ya hifadhin.k
(d)
KILIMO: Wananchi wanaozunguka hifadhi hulima mazao mbali mbali
kama vile tangawizi, vitunguu,iliki,nyanya. Mazao haya ya kilimo wananchi
huwauzia wananchi wengine, wafanyakazi na hata watalii wanaotembelea hifadhi ya
Chome
(e)
UMWAGILIAJI: Hifadhi asilia ya Chome ni chanzo
kikubwa cha maji kwa matumizi ya umwagiliaji wa mazao kama mpunga (mradi wa
Ndungu), tangawizi, iliki,vitunguu, nyanya. Kilimo cha mazao tajwa hapo juu ni
mkombozi wa wananchi katika kujipatia kipato na kuondokana na umaskini.
6.0 CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI HIFADHI
YA MAZINGIRA ASILIA YA CHOME
Kwa sababu ya wananchi wanaozunguka
hifadhi kutegemea hifadhi katika shughuli za kujiongezea kipato, changamoto
zifuatazo zimekwamisha juhudi endelevu za kuhifadhi mfano:
·
Uchimbaji wa madini
ndani ya hifadhi
·
Uchomaji
moto
·
Upasuaji
wa mbao na ukataji miti
·
Uchungaji
wa mifugo ndani ya hifadhi(hii ni kwa kiwango kidogo).
·
Kuwasha
moto makusudi kwa lengo la kukomoana kati ya baadhi ya watu na uongozi wa
kijiji. Mfano watu waliozuiwa kulima mirungi wanawakomoa walima vitunguu na
tangawizi wanaopata maji kutoka kwenye hifadhi ya Chome
·
Faini
ndogo inayotolewa kwa waharibifu wa mazingira na misitu mara wafikishwapo
mahakamani
·
Ushiriki
mdogo wa wananchi katika shughuli za hifadhi hii ikiwa ni pamoja na kushidwa
kuja kutoa ushahidi mahakamani mara wanapotakiwa kufanya hivyo. Aidha baadhi ya
wananchi kukataa kuzima moto kwa kisingizio kuwa jukumu hilo ni la watu wa misitu
·
Wakati
mwingine watumishi kushambuliwa na wananchi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao Mfano doria
7.0 JITIHADA ZILIZOFANYIKA KATIKA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO
ZA UHIFADHI
Pamoja na changamoto hizo hifadhi ya
mazingira asilia kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikifanya jitihada
mbalimbali katika kupambana na changamoto zilizoainishwa hapo juu ambazo zimeonyesha
mafanikio yafuatayo:
·
Kwa
kufanya doria shirikishi tumefanikiwa kuwaondoa wachimbaji wa madini ndani ya
hifadhi. Bado jitihada zinaendelea ili kudhibiti uvamizi huu na kuumaliza
kabisa.
·
Upasuaji
mbao umepungua kutokana na doria shirikishi kati ya watumishi wa misitu na
wananchi. Hii imetokana na elimu ya uhifadhi wa misitu tunayowapa jamii
inayozunguka hifadhi pamoja na uimarishaji wa sheria ya usimamizi wa misitu ya
mwaka 2002 pamoja na sheria ndogondogo za vijiji(Village bylaws)
·
Kuuongeza
ushiriki wa wananchi kwa kuanzisha Kamati za Maliasili za vijiji kwa kila kijiji.ambazo
jumla ni 27.
·
Kuimarisha
mpaka wa hifadhi kwa kupanda miti na kuweka mabango ili kuzuia uvamizi wa
hifadhi.
·
Kuandaa
mipango kazi ya usimamizi wa misitu kwa kila kijiji kinachozunguka hifadhi
asilia ya Chome
·
Kuwawezesha
wananchi kuanzisha bustani zao za miti ili kupanda katika maeneo yao.
·
Kuwahamasisha
wananchi kutokuwasha moto bila sababu na pindi unapotokea kushiriki kikamilifu
kuzima moto.
·
Kutoa
mafunzo kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira
8.0 USHIRIKI
WA WADAU WENGINE KATIKA UHIFADHI
Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Chome
inashirikiana na wadau wafuatao katika kuhakikisha usimaimizi na uhifadhi
endelevu wa hifadhi ya Chome/Shengena
·
Ofisi ya Mheshimiwa Mkuu
wa Wilaya ya Same
·
Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Same.
·
Ofisi ya Mkuu wa kituo
cha polisi Same
·
Mfuko wa hifadhi ya
milima ya Tao la mashariki (EAMCEF)
·
Shirika la ONGAWA
kupitia shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG)
·
Mhifadhi Mkuu wa hifadhi
ya Mkomazi
·
Serikali na Halmashauri
za vijiji
·
Jamii inayozunguka
hifadhi ya Mazingira Asilia ya Chome
9.0 MAPENDEKEZO
Pamoja na jitihada zinazofanywa na
Hifadhi ya Mazingira asilia ya chome pamoja na wadau wengine bado jitihada za
pamoja zinahitajika ikiwa ni pamoja na vyombo vya sheria kama Mahakama kutoa
adhabu kali kwa wahalifu wanaokamatwa ndani ya hifadhi ili iwe fundisho kwa
wengine maana wakati mwingine wanatozwa
faini ndogo ambayo inamfanya alipe mara moja na hivyo kuwafanya wengine kutoona
woga wa kuharibu mazingira.
10.0 HITIMISHO
Umasikini wa kipato kwa jamii ni changamoto kubwa katika shughuli za
uhifadhi wa misitu. Kwa kutumia fursa zilizopo katika jamii inayohusika na kwa
kuunganisha nguvu za pamoja na wadau wote uhifadhi endelevu unawezekana kwa
ajili ya faida ya wana Same na Taifa kwa ujumla.
Comments
Post a Comment