Kuhusu Sisi

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ((Tanzania Forest Services (TFS) Agency)) ulianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali (GN 269) la tarehe 30/7/2010 na kuzinduliwa rasmi tarehe 18/7/2011. Kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala “the Executive Agencies Act Cap. 245 (Revised Edition 2009)”, pamoja na Sera ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria za Misitu na Nyuki Sura 323 na Sura 224 za mwaka 2002. Aidha, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania uliundwa kwa kuzingatia Programu ya Serikali ya Maboresho katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2000 (Public Service Reforms Programme (PSRP 2000)). Programu hii ililenga kuimarisha Idara na Wakala (Ministerial Departments & Agencies (MDAs)) katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora na madhubuti katika utumishi wa umma, ambapo Wakala zinakuwa na uwezo, motisha na mbinu za mabadiliko yenye kuleta ufanisi na tija kiutendaji.  1.1 Lengo Kuu la Kuanzishwa Wakala wa Huduma

Hifadhi ya Mazingira Asilia Chome/Shengena

Hifadhi ya Mazingira Asilia Chome/Shengena inasimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Hifadhi hii ilitangazwa katika tangazo la Serikali (GN) Na. 125 la tarehe 25/05/1951 kama msitu wa Hifadhi. Baadaye hifadhi hii ilipandishwa hadhi na kuwa Hifadhi ya Mazingira Asilia kwa tangazo la Serikali Na. 105 la tarehe 25/03/2016. Hifadhi ina ukubwa wa hekta 14,283 na urefu wa mpaka upatao Kilometa 67. Hifadhi inazungukwa na vijiji 27, kata 11 ambapo wakazi wake kwa kiasi kikubwa maisha yao hutegemea uwepo wa hifadhi ya Chome kwa shughuli za kiuchumi na kijamii. Hifadhi hii ina umuhimu mkubwa Kitaifa na Kimataifa kutokana na vyanzo vingi vya maji vilivyopo na utajiri mkubwa wa bioanuwai. Katika kuhakikisha kuna usimamizi mzuri, hifadhi ya mazingira asilia ya Chome imegawanyika katika maeneo (Safu) matano  ya usimamizi ambayo ni Chome, Suji, Mamba myamba, Bombo na Bwambo.

2.0 MALENGO

 Hifadhi hii imeanzishwa ikiwa na malengo yafuatayo:

1 .Kutunza mazingira asili, mifumoikologia katika uasilia wake.
2. Kuimarisha uhifadhi wa baioanuwai na mifumoikolojia.
3. Kuimarisha mafunzo na tafiti mbalimbali.
4. Kushirikisha jamii na wadau wote katika kulinda, kuhifadhi na kuendeleza
    uhifadhi.
5. Kuelimsha jamii inayozunguka hifadhi njia mbadala ya kujiongezea kipato katika kupunguza umaskini na kupunguza utegemezi wa hifadhi
3.0 UMUHIMU WA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA YA CHOME

Hifadhi ya mazingira asilia ya chome ni hifadhi yenye umuhimu wa kipekee siyo tu kwa wakazi wa wilaya ya Same bali pia  hata kwa Taifa kwa ujumla. Hifadhi hii ina umuhimu ufuatao:-
·         Eneo hili lina bio-anuwai nyingi za mimea na wanyama(ndwele/adimu).   wanaopatikana katika hifadhi hii pekee . mojawapo ya ndege ndwele anaitwa “South Pare white eye”        .

Picha 1: South Pare  White eye. Picha 2: Black and white colobus monkey

·         Hifadhi hii, ni kivutio cha utalii wa wanyama, ndege, maporomoko ya maji, maumbile asilia, mimea adimu nk.

·        Eneo hili linatunza maumbile ya asili,  kuboresha hali ya hewa na kuhifadhi gesi ukaa na kuvuta mawingu yanayoleta mvua za mara kwa mara.













·        Hifadhi hii ni chanzo cha maji kwa matumizi ya kilimo na chakula kwa jamii na wakazi wanaozunguka hifadhi hii



4.0 SHUGHULI ZINAZOTEKELEZWA NA HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA YA CHOME

Ili kuhakikisha kuwa uhifadhi unaendelea na hatimaye kufikia malengo na umuhimu  tajwa hapo juu hifadhi hii inafanya shuguli zifuatazo;

·        Kufanya Doria shirikishi ndani na nje ya Hifadhi kwa kushirikiana na Kamati za Maliasili za vijiji.
·        Kuimarisha mpaka wa hifadhi kwa kusafisha mipaka na kupanda miti kwa lengo la kuepuka wavamizi wa hifadhi na kudhibiti matukio ya moto.
·        Kurejesha maeneo yaliyoharibiwa na wachimbaji madini haramu kwa kufukia mashimo yaliyoachwa wazi, kurudisha mikondo ya maji kwenye njia za asili na kupanda miti.
·        Kuimarisha miundo mbinu ya  kitalii kwa ajili ya utalii ikolojia.
·        Kuiwezesha jamii inayozunguka hifadhi kuanzisha bustani zao za miti  kwa ajili ya kupanda katika maeneo yao.
·        Kuiwezesha jamii inayozunguka  hifadhi kuanzisha miradi midogomidogo ya kujiongezea kipato mfano ufugaji nyuki,ufugaji wa vipepeo, ufugaji wa samaki , ufugaji wa kuku n.k.
·         Kushirikisha jamii katika shughuli za uhifadhi na utunzaji wa mazingira kwa ujumla
·        Kuandaa mipango ya utekelezaji kazi, usimamizi wa hifadhi na sheria ndogondogo za vijiji
·        Kutengeneza mabango yanayoelezea eneo la hifadhi na kuyasimika  katika mipaka ya hifadhi
·        Kuweka maboya kwenye mpaka wa hifadhi ili kudhibiti wahalifu kutoka nje ya  hifadhi ya asilai ya Chome


5.0 FULSA ZA HIFADHI YA CHOME KWA WANANCHI NA JAMII

(a)    UTALII : Katika kuongoza watalii, wananchi wanapata kipato kwa kuongoza watalii, mfano kata ya Chome wananchi wamenufaika kwa kutembelewa na watalii katika nyumba zao na kuona jinsi wanavyoishi kulingana na tamaduni za Kipare. Aidha watalii wameweza kufadhili baadhi ya watoto wa jamii kuwasomesha shule

(b)    UWEKEZAJI: Kuna fursa za kuwekeza kwenye hifadhi kama kujenga hoteli za kitalii, ufugaji nyuki,ufugaji vipepeo, uwekezaji wa kuanzisha umeme mdogo kwenye maporomoko ya maji ndani na nje ya hifadhi, uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vidogo vya maji ya kunywa nk. Aidha wakati wa kujenga miundo mbinu ya utalii mfano hoteli, wananchi wamepata ajira.

(c)    AJIRA: Wananchi wamekuwa na wataendelea kuajiriwa kwa kazi za usimamizi wa hifadhi mfano ufyekeaji wa mipaka ya misitu, usimikaji wa maboya (beacons), parizi za barabara ndani ya hifadhin.k


(d)    KILIMO: Wananchi wanaozunguka hifadhi hulima mazao mbali mbali kama vile tangawizi, vitunguu,iliki,nyanya. Mazao haya ya kilimo wananchi huwauzia wananchi wengine, wafanyakazi na hata watalii wanaotembelea hifadhi ya Chome

(e)    UMWAGILIAJI: Hifadhi asilia ya Chome ni chanzo kikubwa cha maji kwa matumizi ya umwagiliaji wa mazao kama mpunga (mradi wa Ndungu), tangawizi, iliki,vitunguu, nyanya. Kilimo cha mazao tajwa hapo juu ni mkombozi wa wananchi katika kujipatia kipato na kuondokana na umaskini.








6.0  CHANGAMOTO ZINAZOIKABILI HIFADHI YA MAZINGIRA ASILIA YA CHOME

 Kwa sababu ya wananchi wanaozunguka hifadhi kutegemea hifadhi katika shughuli za kujiongezea kipato, changamoto zifuatazo zimekwamisha juhudi endelevu za kuhifadhi mfano:

·        Uchimbaji wa madini ndani ya hifadhi
·        Uchomaji moto
·        Upasuaji wa mbao na ukataji miti
·        Uchungaji wa mifugo ndani ya hifadhi(hii ni kwa kiwango kidogo).
·        Kuwasha moto makusudi kwa lengo la kukomoana kati ya baadhi ya watu na uongozi wa kijiji. Mfano watu waliozuiwa kulima mirungi wanawakomoa walima vitunguu na tangawizi wanaopata maji kutoka kwenye hifadhi ya Chome
·        Faini ndogo inayotolewa kwa waharibifu wa mazingira na misitu mara wafikishwapo mahakamani
·        Ushiriki mdogo wa wananchi katika shughuli za hifadhi hii ikiwa ni pamoja na kushidwa kuja kutoa ushahidi mahakamani mara wanapotakiwa kufanya hivyo. Aidha baadhi ya wananchi kukataa kuzima moto kwa kisingizio kuwa jukumu hilo ni la watu wa misitu
·        Wakati mwingine watumishi kushambuliwa na wananchi wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao Mfano doria



7.0 JITIHADA ZILIZOFANYIKA KATIKA KUPAMBANA NA CHANGAMOTO ZA UHIFADHI
Pamoja na changamoto hizo hifadhi ya mazingira asilia kwa kushirikiana na wadau wengine imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali katika kupambana na changamoto zilizoainishwa hapo juu ambazo zimeonyesha mafanikio yafuatayo:

·        Kwa kufanya doria shirikishi tumefanikiwa kuwaondoa wachimbaji wa madini ndani ya hifadhi. Bado jitihada zinaendelea ili kudhibiti uvamizi huu na kuumaliza kabisa.
·        Upasuaji mbao umepungua  kutokana na doria  shirikishi kati ya watumishi wa misitu na wananchi. Hii imetokana na elimu ya uhifadhi wa misitu tunayowapa jamii inayozunguka hifadhi pamoja na uimarishaji wa sheria ya usimamizi wa misitu ya mwaka 2002 pamoja na sheria ndogondogo za vijiji(Village bylaws)
·        Kuuongeza ushiriki wa wananchi kwa kuanzisha Kamati za Maliasili za vijiji kwa kila kijiji.ambazo jumla ni 27.
·        Kuimarisha mpaka wa hifadhi kwa kupanda miti na kuweka mabango ili kuzuia uvamizi wa hifadhi.
·        Kuandaa mipango kazi ya usimamizi wa misitu kwa kila kijiji kinachozunguka hifadhi asilia ya Chome
·        Kuwawezesha wananchi kuanzisha bustani zao za miti ili kupanda katika maeneo yao.
·        Kuwahamasisha wananchi kutokuwasha moto bila sababu na pindi unapotokea kushiriki kikamilifu kuzima moto.
·        Kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira

8.0 USHIRIKI WA WADAU WENGINE KATIKA UHIFADHI

Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Chome inashirikiana na wadau wafuatao katika kuhakikisha usimaimizi na uhifadhi endelevu wa hifadhi ya Chome/Shengena

·        Ofisi ya Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Same
·        Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same.
·        Ofisi ya Mkuu wa kituo cha polisi Same
·        Mfuko wa hifadhi ya milima ya Tao la mashariki (EAMCEF)
·        Shirika la ONGAWA kupitia shirika la Kuhifadhi Misitu Tanzania (TFCG)
·        Mhifadhi Mkuu wa hifadhi ya Mkomazi
·        Serikali na Halmashauri za vijiji
·        Jamii inayozunguka hifadhi ya Mazingira Asilia ya Chome

9.0 MAPENDEKEZO

Pamoja na jitihada zinazofanywa  na Hifadhi ya Mazingira asilia ya chome pamoja na wadau wengine bado jitihada za pamoja zinahitajika ikiwa ni pamoja na vyombo vya sheria kama Mahakama kutoa adhabu kali kwa wahalifu wanaokamatwa ndani ya hifadhi ili iwe fundisho kwa wengine maana wakati mwingine  wanatozwa faini ndogo ambayo inamfanya alipe mara moja na hivyo kuwafanya wengine kutoona woga wa kuharibu mazingira.


10.0 HITIMISHO

Umasikini wa kipato kwa jamii ni changamoto kubwa katika shughuli za uhifadhi wa misitu. Kwa kutumia fursa zilizopo katika jamii inayohusika na kwa kuunganisha nguvu za pamoja na wadau wote uhifadhi endelevu unawezekana kwa ajili ya faida ya wana Same na Taifa kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

Muundo wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Kuhusu Sisi