Kuhusu Sisi

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ((Tanzania Forest Services (TFS) Agency)) ulianzishwa kisheria kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali (GN 269) la tarehe 30/7/2010 na kuzinduliwa rasmi tarehe 18/7/2011. Kuanzishwa kwa Wakala wa Huduma za Misitu ni kwa mujibu wa Sheria ya Wakala “the Executive Agencies Act Cap. 245 (Revised Edition 2009)”, pamoja na Sera ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998, Sheria za Misitu na Nyuki Sura 323 na Sura 224 za mwaka 2002. Aidha, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania uliundwa kwa kuzingatia Programu ya Serikali ya Maboresho katika Utumishi wa Umma ya mwaka 2000 (Public Service Reforms Programme (PSRP 2000)). Programu hii ililenga kuimarisha Idara na Wakala (Ministerial Departments & Agencies (MDAs)) katika kuhakikisha utoaji wa huduma bora na madhubuti katika utumishi wa umma, ambapo Wakala zinakuwa na uwezo, motisha na mbinu za mabadiliko yenye kuleta ufanisi na tija kiutendaji.  1.1 Lengo Kuu la Kuanzishwa Wakala wa Huduma

SERIKALI YAONYA UNUNUZI WA ARDHI KATIKA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI




Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amewaasa wananchi kutonunua maeneo ya ardhi ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi yanayouzwa na wavamizi.
Akizungumza mwanzoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Prof. Silayo alisema Serikali haijabadili matumizi ya Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi ulioko Kisarawe mkoani Pwani, na kwamba eneo hilo lisikaliwe na raia yeyote au kutumika kwa namna nyingine yoyote kama ilivyotanganzwa na tangazo la Serikali Na. 306 lililochapishwa 24/9/54 AN 4/67/20.
Aliyazungumza hayo mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Usimamizi Rasilimali za Misitu, Bw. Zawadi Mbwambo kuwa kuna watu wamevamia Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi na kuanzisha makazi na wengine wanafanya shughuli nyingine za kibinadamu ikiwemo kuuza viwanja.
Alisema kinachofanywa na wavamizi hao ni kinyume na sheria na Serikali haitawavumilia wale wote waliovamia na kuanzisha makazi ndani ya maeneo ya hifadhi ya msitu na hivyo kuwataka waondoke haraka 
“Kuna watu wanauziwa viwanja kwa bei rahisi katika Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi iliyoko karibu kabisa na makazi ya watu nawaasa wananchi msikubali kutapeliwa! Ukinunua nawe unakuwa mvamizi na TFS na Serikali kwa ujumla haitajali kuwa umepewa hati miliki au la, hilo ni eneo la msitu wa hifadhi na shughuli zozote za kibinadamu haziruhusiwi, utalazimika kuondoka tu.”
Msitu wa Hifadhi wa Kazimzumbi wenye eneo la ardhi lipatalo hekta 12,015, lililopo Wilaya ya Kisarawe Kusini na Kusini – Magharibi ya Boma la Kisarawe, Magharibi ya barabara ya Pugu – Chanika, Kaskazini ya njia ya Chanika – Masaki na Kusini ya barabara ya Dar es Salaam – Morogoro kwa kiasi kikubwa hutumika kuvuta hewa chafu inayotokana na viwanda na mlundikano wa magari ya jiji la Dar es Salaam na mikoa ya karibu yake.
Chini ni tangazo la Selikali la Mwaka 1954 likiutangaza Msitu wa Kazimzumbwi kuwa ni Msitu wa Hifadhi:

TANGANYIKA GAZETTE, Jal. XXXV Na. 54 tarehe 24 Septemba, 1954 
TANGAZO LA SERIKALI NA. 306 LILILOCHAPISHWA 24/9/54 AN 4/67/20 
SHERIA YA MISITU 
(KIF. 132) 
TANGAZO 
(Chini ya sehemu ya 4 ya Sheria ya Misitu) 
TANGAZO LA HIFADHI YA MSITU WA KAZIMZUMBWI 
E.F. TWINING, 
Gavana. 
KWA KUWA MIMI, EDWARD FRANCIS TWINING, Gavana na Amiri Jeshi Mkuu wa Tanganyika, nimeridhika kuwa inafaa kulifanya eneo la ardhi ya umma lililomo ndani ya mipaka iliyoelezwa katika Jedwali iliyoambatanishwa liwe ni hifadhi ya msitu, na kwamba eneo hilo lisikaliwe na raia yeyote au kutumika kwa namna nyingine yoyote. 
HIVYO BASI, SASA, kwa mamlaka niliyopewa katika sehemu ya 4 ya Sheria ya Misitu, nalitangaza eneo lililotajwa kuwa ni hifadhi ya msitu. 
JEDWALI 
WILAYA YA KISARAWE, JIMBO LA MASHARIKI 
Hifadhi ya Msitu wa Kazimzumbwi – Eneo lote la ardhi linalofikia karibu ekari 12,015, lililopo Wilaya ya Kisarawe Kusini na Kusini – Magharibi ya Boma la Kisarawe, Magharibi ya barabara ya Pugu-Chanika, Kaskazini ya njia ya Chanika – Masaki na Kusini ya barabara ya Dar es Salaam – Morogoro (Rejea ya Ramani ya Nchi 1:1,000,000 sheet, Kusini B37 (F VI) kama ilivyofafanuliwa katika Mpango wa Idara ya Misitu Na. JL 196 iliyowekwa katika Idara ya Ardhi na Upimaji na Mipaka yake ni kama ifuatavyo: 
Mashariki – Kuanzia boya Na. 1 kwa upande wa Kusini kwenye njia panda ya Barabara ya Dar es Salaam – Maneromango na njia ya kwenda kwenye kituo cha chini cha pampu ya maji cha Kisarawe futi 1,150 Kusini kufuata njia hii hadi kwenye boya Na. 2; kutoka hapo futi 254 kufuata nyuzi 295 hadi kufikia boya Na. 3 kufuata njia ya bomba la maji kuelekea Kisarawe Bomani; kutoka hapo kwa kulifuata bomba hili kuelekea Kaskazini – Mashariki kwa kukatiza mstari wa maboya unaovuka Mto Pwani kwa futi 7,136 hadi boya Na. 21. Kutoka kwenye boya Na. 21 kufuata uwelekeo wa Kusini kwa kukatiza mstari wa maboya kwa futi 8,135 kuvuka Mto Kakurongo na Mto Zumbwi hadi kwenye boya Na. 35; kutoka hapo kwa kufuata uwelekeo wa Kaskazini – Mashariki kwa futi 2,085 hadi kwenye boya Na. 38; kutoka hapo Kusini – Magharibi kwa futi 7,735 hadi kwenye boya Na. 49 kwa kupitia Magharibi ya kijiji cha Nyeburu. Kutoka boya Na. 49 Kuisini – Mashariki kwa futi 3,185 hadi boya Na. 35, kutoka hapo Kaskazini – Magharibi kwa futi 1,972 hadi boya Na. 55 na kutoka hapo Kusini – Mashariki kwa futi 1,438 hadi boya Na. 56. Kutoka boya Na. 56 Kusini-Magharibi kwa futi 9,021 kuvuka Mto Mzinga na Mto Vikongero hadi boya Na. 64, kutoka hapo Kusini – Mashariki kwa futi 5,044 kuvuka Mto Bulampuka na Mto Nzasa hadi boya Na. 70; kutoka hapo Kusini-Magharibi kwa futi 7,667 hadi boya Na. 79 karibu na kijiji cha Nzasa na futi 214 Kaskazini ya njia ya Chanika-Masaki. 
Kusini:- Kutoka boya Na. 79 karibu na kijiji cha Nzasa kwa mkato kupitia mstari wa maboya kufuata uwelekeo wa magharibi kwa futi 10,104 kuvuka Mto Mnyonde hadi boya Na. 96 kwenye mlima Mnyundo karibu na kijiji cha Maguruwe. 
Magharibi:- Kutoka boya Na. 96 kwenye mlima Mnyundo kwa mkato kupitia mstari wa maboya kufuata uwelekeo wa Kaskazini kwa futi 20,704 kuvuka mto Mwangulinga hadi baya Na. 136 Kusini ya kijiji cha Kazimzumbwi, kutoka hapo bado kwa kufuata uwelekeo huo huo wa Kaskazini kwa futi 4,564 kufuata njia hadi kwenye boya Na. 137; kutoka hapo kwa mkato na kufuata mstari wa maboya kwa futi 1,938 hadi kwenye boya N. 141. Kutoka kwenye boya Na. 141 kufuata uwelekeo wa Mashariki kwa futi 1,942 kufuata njia hadi boya Na. 142; kutoka hapo kwa mkato na kufuata mstari wa maboya Kaskazini Mashariki kwa futi 11,072 kuvuka Mto Zumbwi hadi kwenye boya Na. 157 lililopo zizi la Mvule kwa upande wa Kusini wa Barabara ya Dar es Salaam – Morogoro. 
Kaskazini:- Kutoka kwenye boya Na. 157 lililopo Zizi la Mvule katika Barabara ya Dar es Salaam – Maneromango kufuata upande wa Kusini wa barabara Mashariki kwa futi 2,530 hadi boya Na. 158; kutoka kwenye boya Na. 158 kwa mrengo wa kadiri ya nyuzi 105 kwa futi 891 hadi boya Na. 159, kutoka hapo kwa mrengo wa kadiri ya nyuzi 214 kwa futi 2,325 hadi boya Na. 160; kutoka hapo kwa mrengo wa kadiri ya nyuzi 13.50 kwa futi 2,350 hadi boya Na. 162; hivyo kijiji cha Vazama kipo nje ya hifadhi. Kutoka boya Na. 162 kwa mkato na mstari wa maboya kwa futi 3,576 kwa mwelekeo wa mashariki hadi boya Na. 166 kwa upande wa mpaka wa Magharibi wa shamba la mipira E.P.L 899 (Registered Plan E1 230/6535). Kutoka boya Na. 166 kufuata njia Kaskazini kwa futi 4,276 hadi boya Na. 167 kwa upande wa Kusini ya Barabara ya Dar es Salaam – Morogoro; kutoka hapo kwa upande wa kusini ya barabara Mashariki kwa futi 3,265 hadi boya Na. 1, ambapo ilipoanza hifadhi. 
Sehemu zifuatazo siyo sehemu ya hifadhi ya msitu: 
Sehemu ya ardhi iliyokatwa na kuwekwa maboya ipatayo ekari 170 ijulikanayo kama kijiji cha Obani. 
(ii) Shamba la mipira kadiri ya ekari 255 lililosajiliwa chini ya mpango Na. E1 250/6535. 

Comments

  1. Viwanja vinavyouzwa ndondwe huko chanika vip ni vya misitu au?

    ReplyDelete

Post a Comment

Popular posts from this blog

Muundo wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Kuhusu Sisi